Seventh-Day Adventist Church

Swebo Seventh-day Adventist Church

Menu
Add a Slideshow to see your custom images here

HISTORIA YA SWEBO

HISTORIA YA KANISA LA SWEBO

Kanisa la Swebo lilianzishwa mwaka 1981 na kikundi kidogo cha watu wawili waliopokea ujumbe wa Kiadventista kupitia Masomo ya Sauti ya Unabii kwa njia ya Posta yaliyokuwa yakitolewa Kendu Bay - nchini Kenya. Watu hao wawili ni Mzee Sanga na mzee Malira ambao baadaye walizishirikisha familia zao na kuanza kutunza Sabato ya Bwana yaani Jumamosi hapo hapo kijijini kwao Ntokela. Baada ya muda mrefu wa kuwatafuta waumini wenzao wa Kisabato waumini hao wapya walifanikiwa kumpata mchungaji wa Waadventista Wasabato wa eneo lao ambaye alikuwa kwa wakati huo anaishi Tukuyu mjini akisimamia eneo lote la Wilaya ya Rungwe, Wilaya ya Kyela, na sehemu ya Wilaya ya Ileje. 

Kanisa la Swebo ni Kanisa la Waadventista Wasabato lililo kandokando ya barabara itokayo Mbeya kuelekea Kyela hadi mpaka unaotenganisha nchi ya Malawi na Tanzania. Kanisa hili lipo kwenye kijiji cha Ntokela umbali wa maili 30 kutokea Uyole na maili 10 kutoka Kiwira. Kanisa la Swebo ni miongoni mwa makanisa makongwe ya mtaa wa Kiwira wenye makanisa ya Chibila, Ikuti, Igembe, Syukula Lubwe Buswema, Kipande, Malangali, Kiwira, Moria, Ndaga, Ntokela, Igoma, Nyalwela, na Swebo yenyewe. Kanisa la Swebo na Igembe ndiyo makanisa makongwe yenye historia ya kuzaa makanisa mengine ya mtaa wa Kiwira. Wakati kanisa la Igembe likizaa makanisa ya Ikuti, Syukula, Lubwe, Buswema, na mjukuu wake Kiwira, Kanisa la Swebo peke yake ndilo lililozaa makanisa ya Igoma, Ntokela, Malangali, Kipande,  Ndaga, na Moria, na mjukuu wake Nyalwela. Kanisa la Swebo linafahamika pia kwa kusaidia makanisa mengine yaliyo nje ya mtaa kwa uinjilisti hasa kupitia kwaya yao maarufu na kongwe ya Swebo kwa kufanya uinjilisti ulioleta roho nyingi kanisani kuanzia miaka ya 1980. Swebo wamepeleka injili Makete, Tunduma, Kyela, Ileje, Mbeya hadi mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma.

Kanisa hilo sasa limeamua kujenga jengo la kisasa la kuabudia la ghorofa moja ambalo hapo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuketisha watu wapatao 3,000. Ujenzi huo ulioanza mwaka 2002 ulikuwa na makisio ya kugharimu Tshs. 586,193,800/= (milioni mia tano themanini na sita laki moja na elfu tisini na tatu na mia nane tu), hapo utakapokamilika. Hadi sasa ujenzi huo umegharimu Tshs. 225,351,417/= sawa na asilimia 38.44 ya gharama zote. Kiasi hiki kilichotumika kwa ujenzi hadi sasa kinatokana na michango ya waumini wa kanisa la Swebo ambao wakati ujenzi unaanza walikuwa 835 hii ikijumuisha washiriki waliokuja kutengwa baadaye kwenda makanisa ya Malangali, Kipande, Moria na Ndaga ambao jumla yao ni washiriki 679. Washiriki wa Swebo waliobaki na ambao kimsingi ndiyo wanaoendeleza ujenzi ni 192 ambapo 172 ni walio kwenye kitabu cha ushirika yaani waliobatizwa, 20 walio kwenye darasa la ubatizo na 100 ni watoto walio kwenye shule ya Sabato.

Jengo hilo linalojengwa chini ya usimamizi wa Siwe Building Contractors - Mbeya (makandarasi waliobobea na wanaotambulika kisheria) limefikia hatua nzuri ambapo kuta za chini na jamvi linalotenganisha vyumba vya juu na chini vimekamilika. Kwa kukusaidia kuelewa picha za hatua za ujenzi unaweza kuziangalia kwenye tovuti hii.  Hatua inayoendelea kwa sasa ni kumimina nguzo za kuta za ghorofani na kukamilisha ufyatuaji wa matofali ya kujengea ambayo ni matofali 2,000. Matofali yailiyopo hadi sasa ni 1,393.

Hatua ya awali ya ujenzi ni pale ujenzi utakapofikia kujenga kuta zote na hivyo kubakia upauaji na umaliziaji. Vifaa vilivyobakia ili kukamilisha hatua hii ya ujenzi ni upatikanaji wa mifuko ya simenti itakayotumika kufyatulia tofali, kushindilia nguzo za ghorofani, lenta, na kujengea kuta za ghorofani. Vifaa vingine vinavyohitajika ni nondo za milimita 16, 12, na 8 kwa ajili ya lenta ya kuunganishia kuta za ghorofani. Nondo kwa ajili ya nguzo za ukuta wa ghorofani zilishakamilika. Kifaa kingine kinachohitajika ni mchanga wa kujengea na kufyatulia tofali, na kokoto za kumiminia zege. Pamoja na vifaa hivyo pia inahitajika kwa haraka sana fedha ya kuwalipa wakandarasi kwa hatua ya ujenzi tuliyofikia hadi sasa. Mchanganuo halisi utawekwa kwenye tovuti hii baada ya kukamilisha mahesabu kunakofanywa kwa ushirikiano wa makandarasi na kamati teule ya ujenzi.

Kanisa lilifikia hatua ya kuanzisha ujenzi wa kanisa hili la kisasa ili kukidhi hitaji la ongezeko kubwa la waumini katika kijiji hiki. Kama tulivyosema awali kanisa la Swebo lipo kwenye kijiji cha Ntokela ambacho hadi wakati huu kina makanisa matatu makubwa ya Waadventista Wasabato na ambapo wenye ushirika katika makanisa hayo wanafikia 466 ukiondoa walio kwenye madarasa ya ubatizo watoto na wanaopenda mafundisho yetu ambao wanakisiwa kuwa zaidi ya 1500 namba inayofikia nusu ya waumini wote wa mtaa wa Kiwira. Kijiji cha Ntokela ni mkusanyiko wa wageni kutoka maeneo ya Makete Igoma Malangali, Kipande, Ileje na maeneo mengi ya Tanzania waliofuata kilimo na shughuli zingine za kiuchumi.

Takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la wakazi wa kijiji kiasi cha kuifanya serikali ya kijiji kufikiria kukigawa kijiji ili kupata vijiji viwili. Mazingira haya yanaandaa fursa muhimu kwa Kanisa la Swebo kutumika vizuri hapo litakapokamilika, maana pamoja na kuwa na uwezo wa kuchukua watu wengi kwa wakati mmoja jengo litakuwa na huduma za maktaba na huduma zingine za kisasa ikiwepo studio na kituo cha mawasiliano. Jengo hili pia litatumika kama ukumbi wa mikutano ya kidini inayoendeshwa na kanisa kama makambi, au mikutano mingine ya mtaa.

Kanisa la Swebo linawaomba Wasamaria wema popote walipo kulisaidia kukamilisha ujenzi huu mkubwa na muhimu wenye manufaa kwa kanisa na jamii inayowazunguka. Ieleweke kuwa wajenzi wa jengo hilo hadi hatua hiyo iliyofikia ya 38.44% ni wakulima wa kipato cha chini lakini ambao wamedhamiria kumjengea Mungu nyumba inayolingana na hadhi yake. Kwa kuwa gharama za ujenzi zimekuwa zikiongezeka kwa kasi kubwa kila kukicha na jengo wanaloabudia kwa sasa lipo kwenye mazingira hatarishi (lina nyufa) wanaomba wasamaria wema popote walipo wawachangie fedha za kukamilisha mradi huu kwa hatua hii ya kwanza kwa njia na mawasiliano yafuatayo:-

AKAUNTI YA KANISA LA SWEBO:
Account holder: Swebo Seventhday Adventist Church.
Account #: 038201032685
Bank Type: National Bank of Commerce - (NBC).

MAWASILIANO YA SIMU:
+244766939185 - Simu ya Mzee Kiongozi wa Kanisa la Swebo ndugu Bahati Mensa
+255758034740 - Simu ya Mzee wa Kanisa la Swebo ndugu Anyelwisye Wilsoni
+255764794696 - Simu ya Mhazini wa Kanisa la Swebo ndugu Reuben Safari
+255766714913 - Simu ya Kiongozi wa Majengo wa Kanisa la Swebo ndugu Tito Tweve